Kamua hapa
Sean Paul: Mjamaica anayetabiriwa kuiteka Dar |
|
NaSEAN Paul Henriques ni mwanamuziki wa kimataifa ambaye amekubali kusaini mkataba na Prime Time Promotions ili kufanya onesho moja Dar es Salaam kesho, likiwa linaambatana na maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka.
Mbali na Prime Time Promotions, pia Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) kupitia sigara ya Sweet Menthol (SM), 88.4 Clouds FM, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji cha Guinness, Royal Palm Hotel na Outdoor Advertising zimeshiriki kufanikisha ujio wa mwanamuziki huyo.
Sean Paul ana washabiki lukuki katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania na hapana shaka ujio wake utakuwa na manufaa kwa wasanii wa Tanzania ambao kwao ni nafasi muafaka ya kujifunza mambo mengi kutoka kwake ili wapige hatua katika muziki wa kimataifa.
Sean Paul ni mmoja wa Ma-dj na mwimbaji mahiri wa muziki wa ragga na dancehall ambaye Watanzania wanamsubiri kwa hamu kuona vimbwaga vyake 'live' kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Kijana huyo ni mwanamuziki anayevuma ndani na nje ya nchi yake ya Jamaica kutokana na ufundi na mvuto wa muziki wake unaoshabikiwa zaidi na vijana.
Hapana shaka matarajio ya washabiki wengi wa muziki nchini ni kusubiri kupata uhondo kutoka kwake atakapotumbuiza Diamond Jubilee kesho ambapo anatarajiwa kutua Dar es Salaam mchana akitokea Kenya.
Sean Paul anayefanya shughuli zake za muziki Marekani, juzi usiku alifanya onesho Nairobi, Kenya; jana alitarajiwa kutumbuiza Kampala, Uganda; leo atapiga Mombasa, Kenya kabla ya kutumbuiza Dar es Salaam kesho na Jumatatu atakwenda kuburudisha Lagos, Nigeria.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Prime Time Promotions, Gerald Hando, atakapowasili kesho, Sean Paul atatoa zawadi, kula chakula cha mchana, kucheza na kupiga picha na watoto yatima wa vituo vinne vya CCBRT, Kiwohede, Magomeni na Sinza vya Dar es Salaam katika maadhimisho ya sikukuu ya Pasaka. Pia atatembelea Makumbusho ya Taifa.
Anasema Sean Paul anatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam saa 7 mchana kesho akitokea Kenya kwa ndege ya Kenya Airways akiwa na wasaidizi wake 16.
Alioambatana nao wakiwemo wacheza shoo wanne ni Steve Wilson, Jason Henriques, Jerome Hamilton, Terrence Harold, Laurel Baillie, Richard Foulks, Kenneth Small, Rupert Bent, Duane Summers, Tanisha Scott, Yxia Olivares, Autavia Bailey, Tamara Morrow, Darrell Coles, Donovan Stewart na George Nichailow.
Onesho la Sean Paul litaanza saa 3.30 usiku na atasindikizwa na wasanii wa Tanzania, Salum Makuka 'Sammy Cool', Miss Tanzania 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe, Rehema Chalamila 'Ray C', Jhiko Man, Esther Wasira, Ruta Bushoke, Selemani Msindi 'Afande Sele', Haruna Kahema 'Inspekta Haroun', Juma Kassim 'Juma Nature', Mandojo & Domokaya, Ferouz Mrisho, Braton, Hama Q, AY, Dattaz, Wanne Star na Mez B.
Akizungumzia ujio wa Sean Paul, Meneja wa bia ya Guinness, Ephraim Mafuru anasema anaamini miondoko ya ragga na dancehall anayopiga mwanamuziki huyo itawasaidia wanamuziki wa kizazi kipya nchini kujifunza mengi.
"Guinness iliamua kushiriki kuhakikisha Sean Paul anakuja nchini ili kuwapata fursa wasanii wa kizazi kipya Tanzania kuona mafanikio ya wanamuziki wengine nyota duniani katika soko la kimataifa na kujifunza mengi kutoka kwake.
"Pia tumeona ni wakati muafaka wa kutoa nafasi kwa watu kujaribu kinywaji cha Guinness, ndio maana tumeendesha promosheni kwa watu wa Mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya kupata kuponi ili kuja Dar es Salaam kumuona mwanamuziki huyo ambapo gharama za chakula, malazi na usafiri vinalipwa na Guinness," anasema Mafuru na kufafanua kuwa watu watano watatoka Mbeya, watano Mwanza, kumi Arusha na 20 Dar es Salaam.
Anasema kwa vile Sean Paul ni mnywaji wa Guinness, wamepata msukumo wa kumleta nchini na kudai Guinness iko tayari kuwasaidia wanamuziki nchini kwa kuwasiliana na matawi ya Guinness katika nchi nyingine ili kuwasaidia wasanii wa Tanzania pia kuzuru nchi za nje kufanya maonesho.
Historia yake:
Sean Paul alizaliwa Januari 8, 1973 mjini Kingston, Jamaica, West Indies akitokea katika familia ya kifahari na babu yake mzaa baba alizaliwa Port Antonio, Jamaica.
Asili ya baba yake ni Ureno kwani ana mchanganyiko wa damu ya kireno na kijamaica wakati mama yake ni mchanganyiko wa Mchina na Mjamaica.
Alisoma elimu ya juu ya sekondari katika shule ya Wolmers iliyo karibu na Uwanja wa Taifa wa Mashujaa na kisha akahamia Bel Air High School iliyopo Mandeville.
Akiwa shuleni, alikuwa bingwa katika riadha na michezo ya majini (Water Poll) kupitia timu ya taifa ya Jamaica. Mwaka 1989 na 1991 alishiriki michezo ya Carifta.
Pia alisomea Utawala wa Hoteli katika Chuo cha Sanaa, Sayansi na Teknolojia (Hivi sasa ni Chuo Kikuu cha Teknolojia) kilichopo Hope Road ambapo alipata shahada ya Uongozi wa Hoteli na biashara. Baadaye alifanya kazi katika benki.
Inadaiwa kuwa mama yake alianza kumwandalia mazingira ya fani ya muziki ambapo wakati akiwa na umri wa miaka 13 alimnunulia kinanda. Alikuwa akijaribu kufanya kazi ya u-dj kwenye hafla mbalimbali.
Kutokana na kuwa na msukumo katika dancehall, alianza kuandika nyimbo, japokuwa amepata mafanikio makubwa akiwa mwimbaji na si mtunzi.
Baadaye alianza kujenga uhusiano wa karibu na bendi za Roots Reggae na Third World ambapo alikutana na mzalishaji wa muziki wa ragga muffin, Jeremy Harding.
Wimbo wake wa kwanza 'Baby Girl' alitoa mwaka 1996 na kumfungulia mlango wa mafanikio. Aliendelea kutunga nyimbo nyingine kama 'Deport Them' na 'Infiltrate'. Aliandaa kundi maarufu la Dutty Cup Crew akiwa na Daddigan na Don Yute.
Mwaka 1997, Paul alirekodi akiwa ameungana na Spanner Banner aliyekuwa akitamba Jamaica, ambapo waliimba wimbo wa "Ladies Man", waliourekodi Sweet Angel Productions.
Kibao hicho kilisababisha anyakuliwe na Jeremy Harding, ambaye ni mtayarishaji muziki aliyewahi kufanya kazi na Beenie Man katika wimbo wa "Who Am I". Mtayarishaji huyo ndiye aliyeandaa wimbo wa miondoko ya dancehall wa "Baby Girl", uliofuatiwa na "Infiltrate" uliopata mafanikio makubwa.
Mwaka 1999 aliungana na mwimbaji wa muziki wa ragga muffin, Vegas na rapa DMX kurekodi 'Hot Gal Today'. Wimbo huo pamoja na 'Deport Them' zilimpandisha chati Marekani na kuwa miongoni mwa nyimbo zilizopigwa katika vituo vikubwa vya redio nchini humo.
Mwaka 1999, Paul alizuru Ulaya, Japan na Marekani ambapo aliungana na Mr. Vegas na rapa wa Marekani, DMX na alikonga nyoyo za Wamarekani na wimbo wa "Hot Gal Today" remix na kutoa albamu ya Stage One.
Mwaka 2002, Paul aliingia kwenye Kumi Bora ya Marekani akiwa na wimbo wa "Gimme The Light" na pia alipata mafanikio mwaka uliofuata kwa wimbo wa "Get Busy" kabla ya kushika namba moja Mei akitamba na Dutty Rock uliouza nakala zaidi ya milioni moja Marekani.
Paul katika kipindi hicho aliwafunika wanamuziki wengine waliokuwa wakitamba na vibao vyao, Blu Cantrell (Breathe) na Beyonce (Baby Boy).
Japokuwa sauti yake na staili zinashabihiana na ma-dj wengine wa muziki huo kama Supercat Sean, Shabba Ranks, Slick Rick, Busta Rhymes na KRS One, lakini nyimbo zake zinatajwa kuwa zimejaa maneno ya lugha ya mitaani ya Marekani ambayo ni kivutio kikubwa kwa vijana.
Februari 8, mwaka huu, Sean Paul aliibuka na tuzo tatu ikiwemo ya mwanamuziki bora wa albamu bora ya ragga, rapa bora wa Solo na msanii bora wa kizazi kipya.
Sean Paul pia amewahi kutumbuiza pamoja na Unda Wata video akishirikiana na Buju Banton, Beenie Man, Buccaneer, Machel na General Degree ambapo ulinzi ulikuwa mkali kwenye ukumbi wa Asylum Club mjini Kingston.
Sean Paul mwenye umri wa miaka 29 sasa, amekuwa na mafanikio kisanii mwaka 2003 ambapo alitwaa tuzo ya Grammy Award katika tamasha la 46.
Albamu ya Dutty Rock ndiyo ilimwezesha kupata tuzo hiyo ya 'Albamu Bora ya Ragga', akiwabwaga wanamuziki wenzake wa miondoko ya ragga, Buju Banton aliyewakilishwa na albamu ya Friends For Life, Wayne Wonder (No Holding Back), Burning Spear (Freeman) na Third World (Ain't Giving Up).
Sean Paul mapema mwezi uliopita pia alizawadiwa tuzo ya Gleaner Honour Award kutokana na mafanikio aliyopata mwaka 2003.
Tamasha la Grammy Awards ambalo lilifanyika kwa mwaka wa 46, lilifanyika kwenye ukumbi wa Staples Centre mjini Los Angeles, California, na lilihudhuriwa na wanamuziki na wanasanaa mbalimbali maarufu duniani hasa Amerika Kaskazini.
Mbali na kushinda Grammy Award kwa mara ya kwanza, Sean Paul amejiongezea mafanikio mengine ambapo kwa mwaka 2003 pekee, albamu yake ya pili ya Dutty Rock imefanya vizuri katika mauzo (kwa kuuza zaidi ya nakala milioni mbili) nchini Marekani, wakati wimbo wake wa Get Busy ulipewa tuzo ya dhahabu na Chama cha Kurekodi Muziki Australia (ARIA).
Kutokana na umahiri alionao katika miondoko ya catchy dancehall, Sean amekuwa akitamba kwenye vituo mbalimbali vya televisheni na redio Marekani.
Katika tamasha la MTV Video Music Awards mwaka jana, alikuwa miongoni mwa waliowania tuzo za 'Best New Artiste in a Video' na 'Best Dance Video'. Hata hivyo, hakushinda yoyote kati ya hizo.
Kwenye tamasha la MTV Europe Awards lililofanyika Edinburgh, Scotland, alikuwa miongoni mwa wanaowania tuzo za 'Best New Act', 'Best Song' na 'Best Single' lakini alishinda ya 'Best New Act' pekee.
Alinyakua 'The Source Award' katika 'Albamu Bora ya Ragga' mwaka jana pia, na pia alikuwa miongoni mwa waliowania tuzo katika tamasha la American Music Awards.
finito... |

My Address
Thisis M. Name 1234 N A Street My City, ST 89098
Online Contact Info
johnsmith@coldmail.com
Website
www.johnsmith.freeservers.com
|
Mfalme wa Rhymes: Mashindano yatakayokuza muziki wa hip hop |
|
*Tungo uchwara sasa kupotea *Afande Sele aweka historia
Na Mwandishi Wetu JUMAMOSI wapenzi wa muziki wa hip hop walifurika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee kushuhudia fainali ya mashindano ya kumtafuta mkali wa muziki huo nchini yanayoitwa Mfalme wa Rhymes.
Mashindano hayo yaliandaliwa na kampuni ya Ericom Limited chini ya Mkurugenzi wake, Eric Shigongo na kudhaminiwa na kampuni inayojihusisha na uuzaji wa magari ya Conti Car Sales.
Kufurika kwa wapenzi hao katika ukumbi huo, kulidhihirisha kuwa muziki huo bado una nguvu kubwa nchini kwani baadhi yao walianza kuingia ukumbini saa 12 jioni badala ya saa 3.00 usiku ili wasikose nafasi.
Ni wasanii kumi na wenye heshima kubwa katika muziki wa hip hop nchini ambao walikuwa wanapambana jukwaani kuwania taji hilo.
Wasanii hao ni Juma Kassim 'Juma Nature', Hamisi Mwinjuma 'Mwanafalsafa', Tryphone Ngaiza 'Soggy Dog' ama 'Chief Rumanyika', Haruna Kahena 'Inspekta Haroun', Ferouz Mrisho, Joseph Haule 'Profesa Jay', Msafiri Kondo 'Solo Thang', Selemani Msindi 'Afande Sele' na Juma Mohamed 'Jay Mo'.
Ulikuwa ni mpambano mkali na wa kupendeza, lakini mwisho wa wote Afande Sele kutoka Mji kasoro bahari, Morogoro ndiye aliyeibuka kinara wa mashindano hayo na kuweka historia ya kuwa msanii wa kwanza kunyakua ufalme wa mashindano hayo yatakayofanyika kila mwaka.
Kwa ushindi huo, msanii huyo ambaye anaweka nywele zake katika mtindo wa rasta, amejikwamua katika matatizo ya usafiri kwa kujinyakulia gari dogo na la kisasa aina ya Toyota Cera lenye thamani ya sh. milioni sita.
Msanii huyo alinyakua ubingwa kutokana na nyimbo zake za Mtazamo, Kama Nikipata Ukimwi na Darubini Kali ambao unatamba hivi sasa.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Inspekta Haroun aliyejipatia sh. 300,000 wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na vijana kutoka A Town, Arusha, Mandojo na Domokaya walioshinda sh. 200,000.
Ferouz alishika nafasi ya nne wakati nafasi ya tano ilichukuliwa na Mzee wa mabinti, Mwanafalsafa.
Mashindano hayo ambayo ni ya pili kufanyika katika ramani ya muziki wa hip hop baada ya yale ya Yo! Rap Bonanza yaliyofanyika miaka ya 1990, kwa kiasi kikubwa yamekuza heshima ya muziki huo.
Pia yatachangia maendeleo zaidi ya muziki huo, kwani sasa wasanii watakuwa makini katika kutunga nyimbo ambazo zitaweza kuwaingiza katika kinyang'anyiro hicho cha Mfalme wa Rhymes.
Ni ukweli uli wao wazi kuwa wasanii wengi hivi sasa akili yao ipo kwenye kumiliki magari. Sasa kama kwa kutumia wimbo wako mmoja uliojaa vina vya uhakika, ujumbe mzito kwa jamii, unapata gari, ni vipi usikae chini na kuumiza kichwa kutunga?
Hapo ndipo tutakapoona wale wasanii uchwara na tungo zao zilizojaa ubabaishaji wa hali ya juu, zikitoweka taratibu na kuwaacha wasanii wa kweli na tungo zilizojaa ukweli.
Katika mashindano ya Yo! Rap Bonanza wasanii walikuwa wanashindana uwezo wa kuimba na kumiliki jukwaa, na wasanii wa kweli kama Chief Ramson, Dr Y Thang, marehemu D Robby na kundi la Kwanza Unit walipodhihirisha umahiri wao.
Wasanii kama Joseph Mbilinyi ama Mr II au Sugu, kipindi hicho akijulikana kama II Proud, alionesha kipaji cha hali ya juu katika mashindano hayo hata hivi sasa kupewa heshima kubwa katika muziki huo.
Katika kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanakuwa na nguvu zaidi, Shigongo anasema wanatarajia kuongeza zawadi ili washiriki wote kumi waondoke na chochote.
"Tumeona ni muhimu kila mshiriki wa mashindano haya apate zawadi kama kumbukumbu yake ya kuingia katika mashindano haya," anasema Shigongo.
Anasema pia kampuni yake itaviweka wazi mapema vigezo vinavyotumika katika kumpata bingwa ili kuondoa manung'uniko kwa baadhi ya washiriki kama ilivyotokea mwaka huu.
"Baadhi ya wasanii wanalalamika kutokana na kutovielewa vyema vigezo walivyopewa na badala yake wanakiangalia zaidi kigezo kimoja cha vina. Kwa hiyo ili kuondoa tatizo hili, tutawapa hata semina ili waelewe kabla ya kupanda jukwaani," anasema Shigongo.
Kauli hiyo ya Shigongo iwe chachu kwa wasanii kubadilika na kutunga nyimbo ambazo zitawawezesha kushiriki mashindano hayo mwakani kwa kuzingatia misingi ya muziki huo wa hip hop.
Muziki wa hip hop ambao Wamarekani weusi waliuchukua kutoka Jamaica ni muziki ambao unazungumzia maisha halisi na siku zote umesimama katika kuzungumza ukweli.
finito...
|
|